Home » 2016 July 08 » TCRA yaonya wanaotunza simu zilizozimwa
1:00 AM TCRA yaonya wanaotunza simu zilizozimwa |
Follow @NNurfire ![]() MAMLAKA ya Mawasiliano nchini (TCRA) imewakumbusha wananchi kutoendelea kuwa na simu zilizozimwa majumbani mwao, na badala yake wazipeleke kwa watoa huduma au mamlaka hiyo ili ziharibiwe. Hayo yamebainishwa na Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TCRA, James Kilaba aliyesema si vyema wananchi kuendelea kuwa na simu zilizozimwa kwani zina kemikali zenye madhara. “Niwakumbushe wananchi kutoshikilia simu zilizozimwa majumbani na wanatakiwa kuzipeleka kwa watoa huduma za simu au mamlaka kwa ajili ya kukusanywa na kwenda kuharibiwa,” alisema Kilaba. Aidha, amewaonya wauza vifaa vya mawasiliano vya mkononi na mafundi simu kutobadilisha namba tambulishi za vifaa vya simu za mkononi na kuwa kufanya hivyo wajue ni kosa la kijinai. Kwa mujibu wa kifungu cha 127 cha Sheria ya Mawasiliano ya Kielektroniki na Posta (EPOCA), mtu yeyote anayechakachua simu au laini ya simu kwa lengo la kubadilisha uhalisia wake anatenda kosa ambalo adhabu yake ni faini isiyopungua Sh milioni 30 au kifungo cha miaka 10 jela au vyote kwa pamoja. Kifungu cha 135 cha EPOCA kimeweka adhabu ya faini ya Sh milioni 1.5 au kifungo cha miaka mitano au vyote kwa pamoja kwa mtu atakayekutwa na kosa la kuchakachua simu iliyofungiwa. Kilaba pia amewataka wafanyabiashara wanaoingiza simu nchini wahakikishe simu wanazozileta zinakidhi viwango na zihakikiwe na Shirika la Viwango Tanzania (TBS). Katika hatua nyingine, TCRA imezitaka kampuni za simu nchini kuhakikisha laini za simu zinauzwa kwa wakala anayetambuliwa na mtoa huduma na ambaye ana anuani ya makazi inayofikika na mwenye namba ya utambulishi ya mlipakodi (TIN). Alisema ifikapo Julai 15 mwaka huu, pia kampuni za simu zinatakiwa kuwasilisha orodha iliyohakikiwa ya mawaka wa kusambaza na kuuza laini za simu nchi nzima na kuacha kuwatumia wakala au wasambazaji wasioruhusiwa. |
|
|
| Total comments: 0 | |
